Story by Our Correspondents-
Mratibu wa baraza la vyombo vya habari nchini MCK tawi la Pwani Maureen Mudi amewahimiza wanahabari kuhakikisha wanaangazia taarifa zitakazochangia amani na uwiano wa kijamii humu nchini.
Akizungumza katika Kongamano la amani lililowajiumuisha Wanahabari, Maafisa wa usalama na mashirika ya kijamii mjini Hola katika kaunti ya Tana River, Maureen amesema taarifa zisizozingatia amani na uwiano mara nyingi zimekuwa zikisababisha mizozo ya kijamii humu nchini.
Afisa huyo amewahimiza wadau wote kushirikiana katika utendakazi wao ili kuhakikisha taifa hili linashuhudia amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Kwa upande wao wadau wa masuala ya amani na usalama katika kaunti hiyo wakiongozwa na Ruth Jilo Kase wamesema wako tayari kushirikiana na Wanahabari kueneza jumbe za amani katika kaunti hiyo na pwani kwa jumla.