Licha ya hali kuwa shwari katika chuo kikuu cha Technical University- TUM mjini Mombasa baada ya purukushani la wakati wanafunzi hao walipoandamana kulalamika kuvamiwa na kujeruhiwa na magenge ya kijambazi, sasa madai mapya ya ubakaji yamechipuka kutoka kwa wanafunzi hao.
Baadhi ya wanafunzi wa kike wanaoishi katika eneo la Kisauni wamedai kubakwa juma lililopita na wakawataka Maafisa wa polisi kulisambaratisha genge la kijambazi linaloonekana kuwalenga wanafunzi hao.
Kulingana na wanafunzi hao, magenge hayo ya kijambazi yamekuwa yakiwavamia hasa pindi wanapotoka chuoni nyakati za usiku, kuwajeruhi, kuwaibia na hata kuwabaka Wanafunzi hao.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini la Haki Afrika Bi Salma Hemed ameyataja madai hayo kama mazito mno na akawataka Wanafunzi hao kuripotiwa Shirika hilo ili uchunguzi na hatua zinazostahili kuiidhinishwa.