Chama cha Wamijikenda cha ‘Taireni Association of Mijikenda’ kinataka Mkurugenzi mkuu wa bandari ya Mombasa Daniel Manduku kubanduliwa mamlakani kufuatia azma yake ya kutaka kukata rufaa kuhusu kesi iliyoitisha mkataba wa kubinafsisha eneo la pili la kuegesha makasha katika bandari hiyo.
Mwenyekiti wa Chama hicho Peter Ponda Kadzeha amesema Manduku analenga kuwakandamiza Wapwani kiuchumi hasa kuhusiana na Bandari hiyo ya Mombasa akitaka abanduliwe mamlakani na Mkurugenzi mwengine atakayeliangazia barabara swala la uchumi wa Pwani kukabidhiwa majukumu hayo.
Kulingana na Kadzeha, Manduku amedhihirisha wazi kwamba hana nia yoyote ya kubadilisha hali ya maisha ya Pwani wala kushirikisha Mpwani katika maswala ya kimaendeleo kupitia kwa pato linalopatikana kutoka kwa bandari hiyo ya Mombasa na kamwe hafai kuisimamia bandari hiyo.
Manduku ameweka bayana kwamba atakata rufaa kufuatia uamuzi wa mahakama uliyotaka kusitishwa mara moja kwa mkataba kati ya Serikali ya Kenya na kampuni ya Mediterranean mkataba utakaoikabidhi kampuni hiyo majukumu ya usimamizi wa eneo la kuegesha makasha la ‘Container terminal -2 katika Bandari hiyo ya Mombasa.