Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo akiwa na waliokuwa wafanyikazi wa shirika la utalii la African Safari Club, mbunge huyo ameitaka kamati ya bunge kuhusu maslahi ya wafanyi kazi kuhakikisha wafanyi kazi hao wanalipwa. Picha/ Sammy Kamande.
Taarifa na Sammy Kamande.
Mombasa, Kenya Mei 22 – Waliokuwa wafanyikazi wa Shirika la utalii la African Safari Club wameitaka kamati ya bunge kuhusu maslahi ya wafanyikazi nchini kuingilia kati na kuhakikisha wanapata malipo yao.
Akizungumza kwenye kikao kilichowaleta pamoja wafanyikazi hao na kamati hiyo ya bunge, wafanyikazi hao wamedai kuwa zaidi ya wafanyikazi wenzao 40 waliaga dunia huku wanawao wakikosa masomo.
Akizungumza wakati wa kikoa hicho, Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo ameitaka kamati hiyo kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha wafanyikazi hao wanapata malipo yao ya zaidi ya milioni 298.
“Kwa umri wao na maisha wakachangia utajiri, zikajengwa hoteli nyingi zikatupatia ajira lakini baadaye mambo yakaanza kusabaratika na baada ya hapo kizungu mkuti kikaanza,” amesema Mbogo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo Ali Wario amewaahidi wafanyikazi hao kuwa kamati hiyo itachunguza swala hilo na kuhakikisha haki za wafanyikazi hao zinapatikana.