Story by Hussein Mdune-
Wakulima wadogo wadogo katika eneo la Mavirivirini wadi ya Mwavumbo gatuzi dogo la Kinango kaunti ya Kwale wameitaka Wizara ya Kilimo nchini kuwajumuisha katika bima ya Kilimo.
Kulingana na Saum Bendera Chaka ambaye ni mkulima anayeendeleza kilimo cha Matuta katika eneo hilo amesema mara nyingi wamekuwa wakipata hasara kwa mimea yao na iwapo watajumuishwa katika bima hiyo basi itawasaidia pakubwa.
Saum amesema wamekosa mavuno kwa zaidi ya miaka minne sasa kutokana na uhaba wa mvua huku akidai kwamba endapo bwawa la Mwache litakamilika kwa wakati basi litasaidia pakubwa katika kilimo nyunyizi.
Kwa upande wake Afisa anayeshuhulikia masuala ya utafiti wa Kilimo kutoka Shirika la maendeleo pwani CDA Lorine Riziki amewahimiza wakulima kuzingatia kilimo cha Matuta huku akisema shirika hilo linapania kutoa Tinga ya kuchimba Matuta kwa wakulima wa eneo hilo.