Story by Gabriel Mwaganjoni-
Mgombea wa ugavana wa kaunti ya Kilifi kwa tiketi ya chama cha UDA Aisha Jumwa anazidi kukabiliwa na vikwazo katika safari yake ya kisiasa baada ya wapiga kura wawili kushikilia kwamba hawataondoa kesi mahakamani ya kupinga azma yake ya kuwania ugavana huo.
Wawili hao Rajab Menza na Daniel Chengo Kahindi ambao tayari wamewasilisha kesi katika mahakama kuu ya Mombasa wanasema kwamba wanatilia shaka Shahada ya Aisha Jumwa.
Menza aliyekuwa akiwahutubia wanahabari katika Mahakama ya Mombasa amehoji kwamba uchunguzi wao umebaini kwamba Jumwa hana cheti halali cha Digrii hivyo basi hapaswi kuwania ugavana wa kaunti ya Kilifi.
Menza na Chengo hata hivyo wamekanusha kwamba vita hivyo ni vya kibinafsi na walichukua muda mwingi kabla ya kufika mahakamani ili kukusanya ushahidi wa kutosha kuhusu elimu ya Jumwa.