Taarifa na Alphalet Mwadime
Mombasa, Kenya, Julai 12- Mabinti watatu waliyokuwa wamekwama nchini Qatar baada ya mkataba wao wa ajira kutibuka wamefanikiwa kurudi humu nchini baada ya juhudi za serikali na watetezi wa haki za kibinadamu kufua dafu.
Mmoja wa mabinti hao Kadiwa Mazera amemkashfu vikali wakala aliyefahamika kwa jina la Saddam kwa kuzima mawasiliano licha ya wao kukumbana na madhila hayo.
Kulingana na Kadiwa, pamoja na wenzake Catherine Akinyi na Riziki Mejumaa wamekuwa wakipitia madhila mengi tangu mwezi Mei mwaka huu bila ya mawakala hao kuwasaidia kurudi nyumbani kwao salama.
Akizungumza katika afisi za Shirika la Haki Afrika Mjini Mombasa, Afisa wa maswala ya dharura katika Shirika hilo, Mathias Hezron Shipetta amezidi kuwakosoa mawakala wanaowasafirisha Wakenya kutafuta ajira ughaibuni.
Shipetta hata hivyo anaitaka serikali kuweka mipangilio inayostahili na kuwa na ushirikiano wa karibu kati yake na balozi zake ughaibuni ili kubaini changamoto zinazowakumba wakenya pindi wanapotafuta ajira katika mataifa ya nje na kuzikabili changamoto hizo.