Story by Hussein Mdune–
Kama njia moja wapo ya kuinua viwango vya samaki katika eneo la Tsunza kaunti ya Kwale, wadau wa kimazingira wameanzisha mpango wa upanzi wa miche ya mikoko katika fukwe ya bahari ya Tsunza.
Kulingana na Mwenyekiti wa mradi wa kudhibiti mazingira wa Kazi na Enye, Kamwana Karisa Bengi, tayari wamepanda miche elfu mbili na wanalenga kupanda miche zaidi ya laki moja kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Bengi amewataka wakaazi wa eneo hilo kujitenga na uharibifu wa mikoko na badala yake kujiunga na wadau wa kimazingira kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa upande wake Katibu wa mradi huo Lucy Kazungu amezitaka serikali za kaunti na ile ya kitaifa pamoja na wahisani mbalimbali kuwasaidia na vifaa vitakavyofanikisha upanzi wa mikoko katika fukwe za bahari.