Story by Gabriel Mwaganjoni –
Hali ya wasiwasi inazidi kuwakumba wakaazi wa eneo la Mpeketoni katika kaunti ya Lamu kufuatia ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona.
Naibu Kamisha wa eneo la Mpeketoni Robinson Gakuku amesema katika siku za hivi majuzi wagonjwa wa Corona wawili wamekuwa wakifariki kila siku takwimu ambazo ni za kutisha.
Akizungumza katika eneo la Mpeketoni, Afisa huyo tawala amewakosoa wakaazi kwa kukaidi mpangilio wa kiafya wa kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo, akionya kwamba maafa hayo yataongezeka endapo wakaazi hawatakuwa waangalifu.
Gakuku amesema katika juma hili pekee watu sita wamekuwa wakikimbizwa hospitalini kila siku ili kupokea matibabu ya dharura baada ya kuugua virusi hivyo, huku wale walio katika hali mahututi wakikimbizwa katika hospitali kuu ya King Fahad.
Gakuku amesema Maafisa wa usalama, wale wa utawala na wale wa afya wamezindua mikakati ya kuwalazimisha wakaazi hasa wale wanaokongamana katika masoko kuzingatia masharti yote ya kiafya.