Story by Ephie Harusi –
Idadi kubwa ya wakaazi wa maeneo ya Milore katika eneo bunge la Ganze kaunti ya Kilifi wamenufaika na mradi wa mawasiliano baada ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini CA kujenga mnara katika eneo hilo.
Katibu mkuu msimamizi katika Wizara ya Habari, mawasiliano na tekinolojia nchini Erick Kiraithe amesema mtandao huo utaboresha pakubwa maisha ya wakaazi wa eneo hilo.
Kiraithe amesema serikali itaendeleza mpango huo katika kaunti ya Kilifi ili kuhakikisha maeneo ya mashinani yanaboreshwa zaidi kimawasiliano na mradi huo hauhusika na maswala ya uchaguzi.
Hata hivyo wakaazi wa eneo hilo wakiongozwa na Hinzano Ponda wamesema mradi huo utaboresha zaidi mawasiliano katika maeneo ya mashinani pamoja na biashara zao kwani umetatua changamoto za mawasiliano.
Mradi huo uliofadhiliwa na hazina ya Universial Service fund unalenga pia kunufaisha maeneo ya Gede na Ndugumnani.