Story by Gabriel Mwaganjoni-
Mzozo wa umiliki wa ardhi katika eneo la Maji ya Chumvi eneo bunge la Kinango kaunti ya Kwale umepamba moto huku jamii ya eneo hilo ikisisitiza kwamba ni sharti warudishiwe ardhi yao iliyonyakuliwa.
Wakiongozwa na Askofu wa Kanisa la East Africa Pentecostal Jimbo la Samburu Fredrick Kanato Ndaikwa, jumla ya familia 1,480 zinataka zirudishiwe ardhi yao ya ukubwa wa ekari elfu 60.
Akizungumza na Wanahabari katika eneo hilo Maji ya Chumvi, Kiongozi huyo wa kidini amemsihi rais William Ruto kuhakikisha haki inatendeka na familia hizo zinapata umiliki wa ardhi yao.
Ni kauli iliyopigiwa upato na Mwenyekiti wa wazee wa jamii ya Mwamundu eneo hilo la Maji ya Chumvi, Nyota Mgandi aliyesema ni sharti hati miliki zilizokabidhiwa watu wasiokuwa halisi wa eneo hilo kufutiliwa mbali.
Tayari mzozo huo umefika Mahakamani baada ya Mshirikishi wa utawala kanda ya Pwani John Elungata kuzuru eneo hilo na kuthibitisha kwamba kweli haki ya jamii hiyo ilikiukwa pakubwa.