Story by Ephie Harusi –
Zaidi ya familia 800 katika kijiji cha Nayeni wadi ya Sokoni kaunti ya Kilifi zimeachwa bila makao baada ya makaazi yao kubomolewa usiku wa kuamkia leo.
Kulingana na wakaazi hao, maafisa wa polisi walikivamia kijiji hicho mwendo wa saa sita usiku wa kuamkia leo na kuwabomolea nyumba zao kinyume cha sheria hali ambayo imewaacha katika mahangaiko.
Wakiongozwa na Mwenyikiti wao Mataza Kilumo, wakaazi hao wamesema hakuna agizo lolote la kuwafurusha katika ardhi hiyo yenye ekari 230 iliyotolewa na Mahakama kwani kesi ya ardhi hiyo tayari ilizungumzwa mahakamani bila ya mwafaka wowote.
Kwa upande wao akina mama katika kijiji hicho, wamedai kunyanyaswa na maafisa wa polisi kwa kupigwa na kuumizwa licha ya kuishi katika ardhi hiyo kwa kipindi kirefu bila ya kutatizo na mtu yeyote.
Hata hivyo Wakili George Kithi ametaka hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya maafisa wote waliohusika kuwafurusha wakaazi hao katika ardhi hiyo bila ya kuzingatia sheria, akisema atawasilisha kesi Mahakamani kwa niaba ya wakaazi hao.