Kamati ya maswala ya dharura ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona katika kaunti ya Mombasa imewatahadharisha wakaazi wa kaunti hiyo dhidi ya kupuuza masharti kuzuia maambukizi vya Corona.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho amewataka wananchi kuzingatia kikamilifu masharti yaliotolewa na Wizara ya Afya nchini ili kujilinda na kuwakinga wengine dhidi ya maambukizi.
Hata hivyo Gavana Joho amewaonya wanasiasa kukoma kuingiza siasa katika swala la Covid-19 na badala yake kuwa mstari wa mbele kuwahimiza wananchi kuzingatia kikamilifu masharti ya kujikinga na virusi vya Corona.
Wakati uo huo amewahimiza wakaazi wanaotumia daraja la Liwatoni kuvuka eneo lengine la pili kukumbatia mpango huo kwani kwa kiwango kikubwa daraja hilo lipunguza msongamano ambao umekuwa kishuhudiwa katika kivuko cha feri cha Likoni.
Kwa upande wake Naibu mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Haki Afrika Salma Hemed amewataka wananchi kufuata utaratibu zilizowekwa na serikali kudhibiti msambao wa virusi vya Corona.