Story by Gabriel Mwaganjoni-
Shughuli za kawaida za ujenzi wa bwawa la maji la Mwache katika eneo la Fulugani, gatuzi dogo la Kinango kaunti ya Kwale zimetatizwa baada ya wakaazi kuandamana wakilalamikia ubaguzi katika ugavi wa nafasi za kazi kutoka kwa mradi huo.
Wakiongozwa na Kiongozi wa kijamii Mwambire Haranga, wakaazi hao wamesema licha ya kuahidiwa kwamba wangepewa kipau mbele katika ajira zinazotokana na mradi huo wa kima cha shilingi bilioni 20, wakaazi hao wametupwa nje ya manufaa hayo.
Kulingana na wakaazi hao, ni vyema iwapo Serikali ingewakimu kwa ajira hizo hasa ikizingatiwa kwamba walitimuliwa kwenye mashamba yao na baadhi yao kulipwa fedha kidogo hadi shilingi elfu 250 pekee.
Kwa upande wake, muathiriwa wa mradi huo Nzala Nyiro amesema ni kinyume kwa watekelezaji wa mradi huo ambapo ni Serikali kuu na benki ya dunia kuwabagua wakaazi ilhali wanafahamu vyema kwamba wakaazi hao walipoteza mashamba yao sawa na raslimali zao zote.
Hata hivyo, Kaimu Afisa mkuu wa bodi ya usambazaji maji kanda ya Pwani Martin Tsuma amesema hali hiyo imechangiwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaowachochea wakaazi hao kutatiza mradi huo.
Mradi huo wa ujenzi wa bwawa la Mwache ulipasishwa mwaka wa 2018 na ulianza rasmi Februari 15 mwaka huu japo umegubikwa na utata kuhusu swala la fidia kwa waathiriwa.