Wahudumu wa Matatu mjini Kwale wametishia kuongeza nauli wakati wowote kuanzia sasa kufuatia ongezeko la bei ya mafuta kote nchini.
Akiongea na mwanahabari wetu katika kituo cha magari mjini humo, mmoja wa wanachama wa muungano wa wahudumu wa Matatu mjini humo Omar Mwalauli, amesema kuwa abiria wanaosafiri kutoka Kwale kuelekea Ferry watalazimika kulipa shilingi 150 kutoka bei ya awali ya shilingi 100.
Hata hivyo baadhi ya wakaazi wamewataka wahudumu hao kuwajali abiria, huku wakipendekeza nyongeza ya shilingi 10 kwa nauli ya kila kituo.
Wauzaji wa mafuta wamesema kuwa bei mpya ya mafuta ilianza kutekelezwa hapo jana, lita ya mafuta ya petroli ikiongezeka kwa shilingi 14 na kuuzwa kwa shilingi 124 huku lita ya mafuta ya disel ikiongezeka kwa shilingi 13.
Taarifa na Michael Otieno.