Story by Ali Chete-
Muungano wa Wahudumu wa Afya katika kaunti ya Mombasa umetishia kuelekea Mahakamani na kuishtaki serikali ya kaunti hiyo kwa kukosa kuwalipa mishahara yao ya miezi miwili.
Katibu mkuu wa Muungano huo Franklin Makanga amesema licha ya kuishinikiza serikali ya kaunti hiyo chini ya uongozi wa Gavana Ali Hassan Joho kuwalipa mishahara yao, serikali hiyo imekaidi kutekeleza jukumu lake.
Makanga amesema kwa miaka mingi wahudumu wa afya wamekuwa wakinyanyaswa haki zao huku akidai kwamba Wahudumu hao hawatarudi kazini hadi pale serikali ya kaunti hiyo itakaposhughulikia maslahi yao.
Kauli ya Makanga imeungwa mkono na Katibu wa Muungano wa maabara katika kaunti hiyo Moses Maingi aliyemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati swala hilo.