Story by Ali Chete –
Hatimaye wahudumu wa afya katika kaunti ya Mombasa wamefutilia mbali mgomo wao uliyoratibiwa kuanza rasmi siku ya Jumanne baada ya kulipwa mishahara yao ya miezi miwili.
Kulingana na Katibu wa Chama cha madaktari nchini KMPDU tawi la ukanda wa Pwani Dkt Nassir Shaban, mgomo huo uliyokuwa utawahusisha madaktari, wauguzi, maafisa wa Kliniki sawa na wale wa maabara katika hospitali na zahanati zote za umma katika kaunti hiyo umesitishwa baada ya Serikali ya kaunti ya Mombasa kuwalipa mishahara yao sawa na marupurupu yao yote.
Akiwahutubia Wanahabari katika kaunti ya Mombasa, Dkt Nassir amesema Serikali ya kaunti hiyo imelishughulikia swala lao la hazina ya matibabu NHIF sawa na kulipa mikopo yao katika benki kwa kuambatana na matakwa ya benki hizo.
Nassir aidha amesema swala la kupandishwa vyeo la baadhi ya maafisa hao litaanza rasmi wiki ijayo huku akisema marupurupu ambayo walikuwa hawajalipiwa serikali hiyo imeweza kulipa kwa sasa.
Hapo awali, wahudumu hao wa afya waliapa kulemaza shughuli zote za kimatibabu katika hospitali na zahanati zote za umma katika kaunti hiyo endapo Serikali ya Mombasa haingewalipa mishahara yao kufikia jioni ya leo.