Wafanyibiashara wawili wametozwa dhamana ya shilingi milioni 10 au pesa taslimu shilingi milioni 3 kila mmoja baada ya kukabiliwa na madai ya kukwepa ushuru.
Mahakama imeelezwa kwamba Abdisalam Abdullahi Gedi na mwenzake Yahye Elias Bare wakiwa Wakurugenzi wa kampuni ya uchukuzi ya Liban Trading Limited walikwepa kulipa ushuru kwa mamlaka ya ushuru nchini licha ya kukusanya kima cha shilingi milioni 740.1 katika kipindi cha miaka mitatu katika biashara yao.
Wakili wa mamlaka ya ushuru nchini KRA Moses Ado, ameiambia mahakama kwamba wawili hao pamoja na mshukiwa wa tatu Mohammed Hassan Ali, licha ya kupata pato la shilingi milioni 329.9 kufikia mwezi Juni mwaka wa 2013, na kukusanya shilingi milioni 146.2 mwaka wa 2014 sawa na pato la shilingi milioni 263.9 mwaka wa 2015 hawakulipa ushuru wowote.
Ado amesema wasimamizi hao walikuwa wakijaza alama ya sufuri kwenye nakala maalum za ushuru za mamlaka hiyo ndipo wakaandamwa na maafisa wa ujasusi na kutiwa nguvuni.
Wawili hao wamekanusha mashtaka hayo na mbele ya Hakimu mkuu wa mahakama ya Mombasa Edna Nyaloti huku kesi yao ikiratibiwa kuanza kusikizwa tarehe 8 mwezi ujao wa Novemba.