Jumla ya Wafanyibiashara na makampuni 160 kufikia sasa yamethibitisha kushirikia maonyesho ya kilimo ya mwaka huu Mjini Mombasa.
Kulingana na Mwenyekiti wa Chama cha kilimo ‘Agricultural Society of Kenya’ tawi la Mombasa Bi Anisa Abdallah, wanatarajia kabla ya kukamilika kwa maandalizi ya maonyesho hayo zaidi ya wafanyibiashara 200 watakuwa wamethibitisha kuonyesha bidhaa na huduma zao wakati wa maonyesho hayo.
Akiwahutubia wanahabari katika uwanja wa Mkomani ambapo maandalizi ya maonyesho hayo yameshika kasi, Bi Abdallah amewarai wananchi wote kushiriki maonyesho hayo ili kujionea na kujisomea mbinu mbalimbali za kilimo, ufugaji na huduma nyinginezo mbalimbali msingi na muhimu kwao.
Anisa ameyataja maonyesho ya uvuvi mwaka huu kama tofauti na kipengele kipya kabisa cha uvuvi kujumuishwa kwenye maonyesho hayo, akisema wavuvi watashiriki mashindano ya uvuvi, wageni watapata fursa ya kutazama samaki wakiwa hai kwenye vidimbwi na pia kupata mlo wa samaki.
Maonyesho hayo ya kilimo ya mwaka huu yanayoanza tarehe 4 hadi tarehe 8 Mwezi Septemba mwaka huu yamewavutia wawekezaji wa humu nchini na wale wa kimataifa huku kauli mbiu ikiwa ‘Kukumbatia ubunifu na teknolojia katika kilimo na biashara’.