Story by Correspondents-
Wadau wa maswala ya elimu kaunti ya Mombasa wameitaka Serikali kuhakikisha wanafunzi wa gredi ya sita wanasalia katika shule zao baada ya kukamilisha mtihani wao wa kitaifa wa KPSEA.
Mwenyekiti wa chama cha walimu nchini KNUT tawi la Kilindini Ahmed Kombo Ahmed amesema wanafunzi wa gredi ya sita bado wako na umri mdogo jambo ambalo linawatia hofu wazazi iwapo wanafunzi hao wataungana na wenzao wa shule za upili ambao umri wao umezidi.
Kombo aidha amesema licha ya baadhi ya shule za binafsi kujitahidi kujenga madarasa ya Junior Secondary bado hayatoshi ikizingatiwa kwamba kuna shule ambazo zina idadi kubwa ya wanafunzi wa gredi ya sita ikilinganishwa na shule za upili.
Kwa upande wake mdau wa elimu kaunti ya Mombasa Dan Aloo amesema japo mtaala mpya wa elimu unalenga kuboresha mfumo wa elimu nchini ni lazima serikali iwaajiri walimu wa kutosha.