Kwa mara nyingine tena viongozi wa Kaunti ya Mombasa wamepinga vikali hatua ya serikali ya kuidhinisha makasha yote kusafirishwa kupitia barabara ya reli ya kisasa ya SGR hadi Jijini Nairobi.
Wakiongozwa na Mbunge wa Jomvu Badi Twalib viongozi hao wanasema hatua hiyo imelemaza shughuli za kibiashara na uwekezaji kwa wamiliki wa makampuni ya malori katika Kaunti hiyo.
Akizungumza katika eneo bunge lake la Jomvu , Badi anasema kwamba kamwe hatua hiyo haifai na wawekezaji hawapaswi kulazimishwa kusafirisha makasha yao kupitia barabara ya reli ya kisasa.
Kulingana na Badi hatua hiyo imepelekea wamiliki wa makampuni ya malori kufunga biashara zao hali ambayo vile vile imepelekea maelfu ya Wakaazi wa Kaunti hiyo kupoteza ajira.