Story by Mimuh Mohamed-
Viongozi wa vyama vya WIPER, ANC na Ford-Kenya wamefanya kikao cha pamoja na kutia saini barua ya kujiondoa rasmi katika Muungano wa NASA.
Akizungumza baada ya kikao hicho cha faragha, Kinara wa ANC Musalia Mudavadi amesema wataziwasilisha barua hizo kwa msajili wa vyama vya kisiasa ili kuidhinisha kujiondoa kwa vyama hivyo katika muungano huo.
Kwa upande wake Kinara wa Chama cha WIPER Kalonzo Musyoka amesema kwa sasa wanaangazia zaidi Muungano mpya wa One Kenya Alliance na watazuru maeneo yote ya taifa hili kuuza sare za muungano huo.
Kalonzo aidha amesema muungano wa One Kenya Alliance umelipa kipaumbele suala la kuinua uchumi wa taifa hili ili kuhakikisha wakenya wanajikwamua kutoka kwa umaskini.
Naye kiongozi wa chama cha Ford-Kenya Moses Wetangula amevitaka vyombo vya habari kuwa huru kwa kuwapigia debe wagombea waadilifu badala ya kuwaangazia wanasiasa wasiokuwa na maono kwa taifa hili.