
Mshirikishi mkuu wa usalama kanda ya Pwani John Elungata/ Picha Gabriel Mwaganjoni.
Idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa inamsaka mshukiwa sugu wa ulanguzi wa dawa za kulevya.
Mshirikishi mkuu wa utawala Kanda ya Pwani John Elungata amesema mshukiwa huyo anayeshirikiana na mwenzake katika maeneo ya Mtongwe huko Likoni amekuwa akikwepa mtego wa kikosi cha kupambana na dawa za kulevya.
Elungata aliyekuwa akizungumza katika eneo la Likoni amehoji kwamba kamwe kikosi hicho hakitalegeza kamba hadi pale kitakapomtia mbaroni mlanguzi huyo na kumuadhibu barabara kwa mujibu wa sheria.
Wakati uo huo, Elungata ameitaka jamii hasa wazee wa mtaa kuwafichua walanguzi kwa kikosi cha kupambana na mihadarati Kaunti ya Mombasa ili wakabiliwe.
Operasheni hiyo ya kuwasaka walanguzi wa dawa za kulevya katika Kaunti ya Mombasa imeingia juma la pili sasa ikiyaangazia maeneo ya Kisauni, Likoni, Changamwe, maeneo ya Majengo na Mji wa kale katika Kaunti hiyo.