Wizara ya Afya nchini imewahimiza wakenya kuwa waangalifu zaidi dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwani ni hatari kwa wagonjwa wanaougua maradhi ya kifua kikuu yaani TB, Kisukari na shinikizo la damu mwilini.
Akizungumza na Wanahabari katika jumba la Afya kule jijini Nairobi, Katibu mkuu msimamizi katika Wizara hiyo Dkt Rashid Aman, amesema kila mwaka watu milioni 1.5 huaga dunia kutokana na ugonjwa wa TB.
Akigusia takwimu za maambukizi ya Corona, Dkt Aman, amesema kufikia sasa watu 6,366 wameambukizwa virusi hivyo baada ya watu 176 kupata maambukizi hayo katika muda wa saa 24 zilizopita kutokana na sampuli 2,419 zilizofanyiwa uchunguzi.
Dkt Aman amesema kati ya watu hao 176, watu 100 ni wanaume na 76 wakiwa wanawake na wana umri wa miaka mitatu hadi 76 na wote ni raia wa Kenya.
Hata hivyo amedokeza kuwa kaunti ya Nairobi imenakili visa 99, Mombasa visa 20, Kiambu visa 17, Migori visa 13, Uasin Gishu visa 10, Kajiado na Busia zikinakili visa 4 kila kaunti, huku kaunti ya Kilifi ikinakili visa 3 na kaunti ya Narok, Kakamega na Kisumu zikinakili kisa kimoja kila kaunti.
Wakati uo huo amedokeza kuwa watu 26 wamethibitishwa kupona virusi hivyo na idadi hiyo kuongezeka hadi watu 2,039 huku watu wanne wakiaga dunia na idadi ya waliofariki kufikia watu 148.