Story by Hussein Mdune –
Muungano wa Azimio la umoja umezidi kuwahimiza wananchi wa kaunti ya Kwale kujitokeza kwa wingi na kujisajili kama wapiga kura wakati zoezi hilo lilizinduliwa na Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC likitamatika siku ya Jumapili ya tarehe 6 mwezi Februari.
Viongozi wa Muungano huo katika kaunti ya Kwale wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama cha ODM kaunti ya Kwale Hassan Mwanyoha wamesema hatua hiyo itachangia idadi ya wapiga kura wapya kuongezeka.
Hata hivyo viongozi hao akiwemo Mshirikishi wa chama cha ODM kaunti ya Kwale Nicolas Zani amewahiza vijana ambao hawana vitambulisho vya kitaifa kujitokeza na kuchukua vitambulisho hivyo sawa na kujisajili kama wapiga kura.
Kwa upande wake Mjumbe maalum katika bunge la kaunti ya Kwale Fatuma Masito na Seneta maalum Agnes Zani wamewataka wanawake na vijana kukumbatia zoezi la usajili wa wapiga kura na kujiandikisha.