Mshirikishi mkuu wa utawala kanda wa Pwani John Elungata amewahimiza viongozi wa kaunti ya Lamu kushirikiana na idara ya usalama kupiga vita ugaidi.
Elungata amesema miradi mingi ya serikali inaendelezwa katika kaunti ya Lamu, na iwapo usalama wa kaunti hiyo hautaimarishwa basi huenda ikalemaza juhudi za kutekeleza miradi hiyo.
Akizungumza mjini Mombasa, Elungata amesema ushirikiano huo utasaidia kuimarisha usalama kaunti ya Lamu na kuhakikisha jamii inawadhibiti vijana kutoshauriwa vibaya na baadhi ya watu walio na malengo potovu.
Wakati uo huo amepinga madai yalioibuliwa kuwa kuna baadhi ya maafisa wa polisi wanaoshirikiana na wanasiasa na mabwenyenye kunyakua ardhi za umma.
Haya yanajiri baada ya aliyekuwa gavana wa kaunti ya Lamu Issa Timamy kudai kuwa kuna baadhi ya viongozi wanashirikiana na maafisa wa usalama ndani ya kaunti hiyo kunyakuwa ardhi za umma.
Taarifa na Hussein Mdune.