Maafisa wakuu wa polisi katika Kaunti ya Lamu, wale wa Utawala, Wawekezaji na Viongozi wa kisiasa watachunguzwa kikamilifu na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuhusishwa pakubwa na dhuluma dhidi ya binadamu katika Kaunti ya Lamu.
Mkuu wa sheria nchini Paul Kihara Kariuki ameliamuru Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu la Haki Afrika miongoni mwa Mashirika mengineyo kumkabidhi ripoti zote za dhuluma dhidi ya binadamu zinazotekelezwa katika Kaunti ya Lamu ili awachukulie hatua wahusika.
Kihara amesema kwamba haimakiniki kwa Maafisa wa umma kushirikiana na mabwenyenye katika kuwahangaisha Wakaazi hasa kuhusiana na maswala ya ardhi na kuwatendea madhila mangineyo akisema kwamba ataviandama visa vyote vya dhuluma dhidi ya Wakaazi wa Kaunti hiyo ili wapate haki.
Akiwahutubia Wakaazi wa eneo la Mpeketoni Kaunti hiyo ya Lamu mapema leo, Kihara amesema kwamba ni aibu kwa Maafisa wa umma kushirikiana na wanyakuzi wa ardhi ili kuwahangaisha Wakaazi akisema kwamba tayari amepokea ripoti za dhuluma zinazowahusisha Maafisa wa polisi akisema kwamba wataadhibiwa ipasavyo.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.