Story by Gabriel Mwaganjoni –
Mzozo wa ardhi umezuka upya katika eneo la Maji ya Chumvi Gatuzi dogo la Kinango kaunti ya Kwale huku wakaazi wa eneo hilo wakiwalaumu baadhi ya viongozi kwa kuchochea mgogoro huo.
Wakiongozwa na Kasisi wa Kanisa la Kipentekoste la East Africa Pentecostal jimbo la Samburu Fredrick Ndaikwa, wakaazi hao wamesema wamehangaishwa mno na viongozi kwa takriban miaka minane sasa.
Akizungumza katika eneo hilo la Maji ya Chumvi, Kasisi Ndaikwa amesema utata huo unazidi kuchemka na ni sharti shughuli zote za ujenzi katika eneo hilo zisitishwe.
Kwa upande wake, mmoja wa wakaazi wa eneo hilo Mohammed Yama amesema kuna ulaghai mkubwa unaoendelezwa na baadhi ya viongozi wakishirikiana na maafisa wa serikali kwa lengo la kuwanyang’anya wakaazi ardhi zao.
Hata hivyo, Mshirikishi mkuu wa utawala kanda ya Pwani John Elungata amesema anafanya kila juhudi kuutanzua mgogoro huo wa ardhi uliyodumu tangu mwaka wa 2014.
Japo jumla ya hati miliki 500 zinanuiwa kukabidhiwa wakaazi wanaoishi kwenye ardhi hiyo iliyo na ukubwa wa zaidi ya ekari elfu 60, huku wakaazi wakisema hati miliki hizo ni chache na wengi watakosa.