Viongozi wa kidini katika kaunti ya Mombasa wamewakosoa wanasiasa kwa madai ya kukosa kuyaangazia maswala msingi yanayomhusu mwananchi.
Wakiongozwa na Askofu mkuu wa Kanisa la Ushindi Baptist eneo la Likoni Joseph Maisha, Viongozi hao wamesema wanasiasa wamedhihirisha tamaa ya mamlaka badala ya kuyawajibikia majukumu yao mashinani.
Askofu Maisha amekosoa tabia ya wanasiasa hao akisema imechangia athari nyingi kwa mwananchi huku akiwatahadharisha wananchi dhidi ya kushirikiana na wanasiasa hao.
Mhubiri huyo dini ya kikristo amesema wanasiasa ndio wamechangia hali tata na ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona humu nchini, akiwataka wananchi kupuuzilia mbali sera za viongozi hao kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.
Akigusia masuala ya uhalifu, Askofu Maisha ameitaka Idara ya usalama kuyakabili magenge ya kihalifu yanayowahangaisha wakaazi wa eneo la Likoni na kuimarisha usalama.
Kiongozi huyo wa kidini ambaye pia ni Mwenyekiti wa baraza la Maaskofu katika Ukanda wa Pwani amewakosoa baadhi ya wakaazi wa eneo hilo kwa kuwaficha wahalifu.