Story by Janet Shume-
Viongozi wa baraza la makanisa nchini NCCK tawi la Pwani wamefanya kikao na viongozi mbalimbali wa kike kaunti ya Kwale kujadili changamoto zilizowakumba katika uchaguzi na jinsi wanavyoweza kuzikabili siku zijazo.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa baraza hilo kanda ya Pwani Askofu Peter Mwero viongozi hao wamesema baraza hilo limekuwa likishirikiana kwa karibu mno na viongozi wa kike kupitia mradi wa Wadada wa Pawa ili kuwajenga uwezo.
Kiongozi huyo wa kidini amewahimiza viongozi wote wa kike kaunti ya Kwale na pwani kwa ujumla hususan wale ambao hawakufaulu kushinda katika nyadhfa za kisiasa kujitahidi zaidi ili kuwania nyadhfa za juu zaidi siku za usoni.
Kwa upande wake Edah Wamboi, kiongozi wa wanawake katika baraza hilo kaunti ya Kwale, amesema kupitia mradi huo wa Wadada wa Pawa jamii imeweza kupata mafunzo na kukumbatia uongozi wa wanawake.
Hata hivyo viongozi mbalimbali waliohudhuria kikao hicho wakiongozwa na aliyepigania uwakilishi wanawake kaunti hiyo Bibi Masha,wamelitaka baraza hilo kuendelea kuwashika mkono viongozi wanawake ili kuwajenga uwezo.