Story by Our Correspondents-
Viongozi wa kidini nchini wamesisitiza haja ya wananchi kujitenga na siasa za virugu na badala yake kuwa mstari wa mbele kueneza ujumbe wa amani kote nchini.
Viongozi hao wakiongozwa na Askofu wa Kanisa katoliki jimbo la Mombasa Martin Kivuva, wamesema ili taifa hili lipige hatua kimaendeleo na demokrasia ni sharti wananchi wadumishe amani.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa Askofu Kivuvi, amesema kama viongozi wa kidini wataendelea kuwahimiza wakenya kutambua umuhimu wa amani sawa na kujitenga na vishawishi vibaya.
Kiongozi huyo wa kidini amewaonya wanasiasa dhidi ya kuwachochea wananchi na kufarakana kwa ajili ya maslahi yao binafsi na kuwataka kuwa kieleleza bora kwa jamii kwa kuhakikisha wanawaunganisha wananchi ili kuwe na amani.
Hata hivyo amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi na kushiriki uchaguzi mkuu, akisema kwa kufanya hivyo ndio kutampa mwananchi fursa ya kumchagua kiongozi anayemtaka.