Picha kwa hisani –
Aliyekuwa mbunge wa Likoni Mwendazake Masoud Mwahima anatarajiwa kuzikwa muda wowote kuanzia sasa nyumbani kwake huko Vyemani eneo bunge la Likoni kaunti ya Mombasa.
Viongozi mbali mbali nchini wametuma rambi rambi zao ambapo rais Uhuru Kenyatta amemtaja mwendazake mwahima kama kiongozi mcheshi na aliyejizatiti kufanikisha maenedeleo kwa wananchi wake.
Rais Kenyatta vile vile amemtaja marehemu mwahima kama kiongozi aliyepigania uidhinishwaji wa miradi ya maendeleo katika jamii na mzee alijitoa kuwapa ushauri wa busara wakaazi wa likoni na Mombasa kwa jumla kwa miaka mingi.
Wengine waliotuma rambi rambi ni kinara wa ANC Musalia Mudavadi na gavana wa Mombasa Ali hassan Joho ambao wamemtaja mwendazake kama kiongozi aliyepigania maslahi wa wakaazi wa Likoni na Mombasa kwa jumla.
Naye mwenyekiti wa chama cha WIPER Balozi Chirau Ali Mwakwere amesema kifo cha mwahima ni pigo kwa wapwnai akimtaja mwendazake mwahima kama kiongozi aliyependa maendeleo
Naye mbunge wa sasa wa Likoni Bi Mishi mboko amemtaja mtangulizi wake marehemu Mwahima kama kiongozi muadilifu na aliye wawakilisha vyema wakaazi wa eneo bunge la Likoni alipokua mamlakani.
Kulingana na maelezo ya mwanawe Juma Mwahima, mwendaza ameaga dunia mwendo wa saa tano usiku kutokana na maradhi ya pumu akiwa nyumbani kwake huko vyemani.
Mwahima alichaguliwa kwa mara ya kwanza kama mbunge wa Likoni kupitia chama cha ODM mwaka 2007 na kuchaguliwa kwa awamu ya pili mwaka 2013 ,kabla ya kuhama 0DM mwaka 2016 na kujiunga na chama tawala cha Jubilee ambapo kwenye uchaguzi wa mwaka 2017 alipoteza kiti cha ubunge na nafasi hio kuchukuliwa na mbunge wa sasa Bi Mishi Mboko.
Kabla kuchaguliwa kama mbunge mwendazake Mwahima alihudumu kama Kansela wa eneo la shika adabu,pia alihudumu kama naibu meya wa Mombasa na kuhudumu kama meya wa Mombasa mwaka 1999 hadi mwaka 2002.
Marehemu Mwahima pia aliwahi kuwa mwenye kiti wa chama cha KANU katika eneo la Likoni wakati akianza safari yake ya kisiasa.