Story by Gabriel Mwaganjoni-
Wazee wa mitaa na viongozi wengine wa kijamii wamehimizwa kuandaa vikao vya mara kwa mara vya kijamii mashinani ili kuwawezesha wanajamii kuregelea maadili na mshikamano miongoni mwao.
Afisa wa maswala ya dharura katika Shirika la MUHURI Francis Auma amesema hali inayoikumba jamii kwa sasa ni tatanishi ambapo swala la watu kuuwana, ndoa kuvunjika na watoto kuhangaika yamekuwa matukio ya kawaida katika jamii.
Akizungumza katika eneo la Changamwe kaunti ya Mombasa, Auma amesema ni sharti jamii izingatie muongozo wa kidini na viongozi wenyewe wa kijamii wachukue jukumu la kuandaa vikao vya mara kwa mara vya kifamilia ili kuzuia maovu.
Auma alikuwa akiliangazia tukio la hivi majuzi katika eneo la Mwagosi kule Magongo mwisho kaunti ya Mombasa ambapo mwanamume mmoja anadaiwa kumnywesha sumu mtoto wa Jirani yake kwa jina Vincent Oduge aliyekuwa na umri wa miaka 11 na mtoto huyo akafariki.