Mombasa Kenya , Juni 6 – Licha ya vijana katika Kaunti ya Mombasa kuidhinishiwa miradi mbalimbali ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi, baadhi ya vijana wamedinda kabisa kuikumbatia miradi hiyo na kushiriki uhalifu.
Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir amewasihi maafisa wa usalama kamwe kutowasaza vijana wanaojihusisha na uhalifu na badala yake kuwakabili barabara kisheria kwani Vijana hao wamewatia hofu Wakaazi na Wafanyibiashara wa Kaunti hiyo.
Akizungumza katika eneo bunge lake la Mvita, Nassir amekariri kwamba japo baadhi ya vijana wamesajili makundi yao na kutafuta usaidizi kutoka kwa afisi za wabunge na zile za serikali ya kaunti hiyo, baadhi yao kamwe hawajajishughulisha na harakati hizo na badala yake kuwavamia na kuwaibia wakaazi.
Kulingana na Nassir, hakuna kiongozi yeyote aliyejitokeza ili kuwatetea wahalifu hao kama wanavyodai Maafisa wa usalama na akaweka wazi kwamba ni sharti vijana hao waandamwe kikamilifu, watiwe nguvuni na kushtakiwa ili kuudhibiti uhalifu katika kaunti ya Mombasa.
Kauli ya Nassir inajiri huku Wakaazi wa Gatuzi dogo la Kisauni hasa wale wanaoishi katika maeneo ya Barsheba, Mwandoni, Mtopanga na Bamburi mwisho wakiishi kwa hofu baada ya magenge ya vijana kuwavamia na kuwaibia huku wakiwajeruhi kwa kuwadunga visu.