Story by Rasi Mangale/Ali Bakari –
Wanaharakati wa masuala ya kijamii katika kaunti za Kwale na Mombasa wamezidi kuwaelimisha vijana kuhusu umuhimu wa kujisajili kama wapiga kura ili kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.
Wakiongozwa na Mwanakombo Jerumani kutoka eneo la Matuga kaunti ya Kwale wanaharakati hao wamesema wanasiasa wanapaswa kuchukua jukumu la kuwaelimisha wafuasi wao hasa vijana kuhusu umuhimu wa upigaji kura.
Naye Mwanaharakati wa masuala ya kijamii katika eneo la Shanzu kaunti ya Mombasa Allan Katana amesema ni lazima vijana wachague viongozi watakaowabunia ajira badala ya kuhadaiwa kifedha.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la ushindi Baptist eneo la Likoni Joseph Maisha ameitaka idara ya usalama nchini kuimarisha usalama wakati huu ambapo kampeni za uchaguzi ujao zimepamba moto.