Taarifa na Gabriel Mwaganjoni
MOMBASA, Kenya, Julai 29 – Miaka mitatu baada ya Kituo cha Radio Kaya kuangazia kuhusu wizi wa vigango kutoka humu nchini na kuuzwa nchi za Ng’ambo hatimaye Vigango hivyo viemanza kurudishwa humu nchini.
Kigango ni sanamu ya mtu aliyekuwa kwenye Baraza la Gohu lililo na majukumu ya kuongoza jamii ya Wagiryama na aliyechongwa kwa mti maalum ujulikano kama ‘Mwanga’ na ambacho hupandwa kwenye kaburi au eneo maalum la boma la familia.
Katika makala Kigango hatarini mwanahabari Dominick Mwambui alielezea jinsi walaghai walivyoiba vigango kutoka kwa vigojo na kuviuzia watalii.
Katika makala hayo wazee wa Kaya wakiongozwa na muungano wa Utamaduni wa Malindi (MADCA) waliitaka wizara ya utalii kufanya kila juhudi ili kurudisha vigango hivyo.
Hivi leo katika makavazi ya Fort Jesus Wazee wa Kaya hapa Pwani wamebubujikwa na machozi baada ya kukabidhiwa vigango hivyo katika hafla iliyoongozwa na Waziri wa Michezo, tamaduni na turathi za kitaifa Balozi Amina Mohammed. Wazee hao wakiongozwa na Mzee Kazungu Hawe Risa wamekabidhiwa jumla ya vigango 30.
Kwa upande wake, Katibu wa chama cha kitamaduni cha Malindi District Cultural Association-MADCA Joseph Karisa Mwarandu ameitaja hatua hiyo kama kubwa ya kuhifadhi roho za wazee wa baraza la ‘Gohu’ ambalo lina majukumu ya kutunga sheria na kutoa muongozo kwa jamii ya Wagiryama ambazo ziliibwa na Waingereza miaka ya 60 hadi 80 katika maeneo ya Kilifi.
Mwarandu hata hivyo amefichua kwamba kutokana na wizi wa Vigango hivyo vilivyosafirishwa hadi mataifa ya Uingereza na Marekani miaka ya 80 jamii ya Wamijkenda na hasa Wagiryama imehangaishwa na maswala mbalimbali yakiwemo ukame.
Waziri Amina amewahakikishia wazee hao kwamba wizara yake inajitahidi kuvinasua vigango zaidi zilivyoibwa kwao na kusafirishwa hadi Marekani na Uingereza akisema kwamba tayari vigango vingine 29 viko katika uwanja wa kimatifa wa ndege wa Jomo Kenyatta Jijini Nairobi na hivi karibuni vitakadhibiwa wazee hao.
Akizungumzia tukio hilo mwanahabari Dominick Mwambui amelitaja kama la kipekee na kuihimiza wizara ya utalii kuviachilia vigango zaidi vilivyozuiliwa katika nchi za ulaya.