Mamake marehemu John Mutinda aliyejitosa baharini alfajiri ya siku ya Jumamosi na kufariki sasa anadai mwanawe alikuwa akipitia mateso mengi mno kutoka kwa mkewe.
Musangi Mutinda amefichua kwamba Mkewe John kwa jina la Ruth Mueni amekuwa akimdhulumu mumewe na hata kumchoma kwa maji moto mwezi uliyopita na kisha kumshtaki katika kituo cha polisi cha Central Mjini Mombasa ambapo Maafisa wa polisi walimzuilia John kwa siku nne akiwa na vidonda mwilini baada ya kuchomwa na mkewe.
Musangi amefichua zaidi kwamba Mueni anaficha ukweli kuhusu kile kilichomsukuma mwanawe kuendesha gari lake kwa kasi na kuingia katika Bahari hindi ambapo alifariki na mwili wake ukatolewa baadaye sambamba na gari hilo.
Mama huyo akizungumza nyumbani huko Kitui, Kaunti ya Kitui amesisitiza kwamba Mueni ambaye ni mke wa marehemu John na mama wa watoto watatu ni kiini cha kifo cha mwanawe akiwataka Maafisa wa polisi Mjini Mombasa kuidhinisha uchunguzi wa kina kumhusu mwanamke huyo.
Mgogoro huo unazidi kupamba moto huku mwili wa marehemu John aliyekuwa na umri wa miaka 46 ukihifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya kibinafsi ya Jocham Mjini Mombasa.