Story by Gabriel Mwaganjoni-
Utafiti wa hivi punde uliyofanyiwa uongozi wa ugavana katika kaunti ya Mombasa umebaini kwamba huenda wakaazi wengi wa kaunti hiyo wakakosa kushiriki uchaguzi mkuu wa Agosti 9 kufuatia kubanduliwa nje kwa aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko katika kinyang’anyrio cha ugavana wa kaunti ya Mombasa.
Utafiti huo uliyofanyiwa jumla ya wakaazi 4,920 umebaini kwamba wakaazi wengi wa kaunti hiyo walighadhabishwa na hatua ya Tume ya IEBC ya kumbandua Sonko nje ya kinyang’anyiro cha ugavana wa Mombasa na kuamua kutoshiriki uchaguzi huo.
Mtafiti mkuu wa Shirika la utafiti la Research and Governance Professional Organization George Dzombo amesema utafiti huo uliyofanya kwa siku 5 na kutoa matokeo hayo na wakaazi wengi hawajaamua lolote, huku wengine wakimuunga mkono Hassan Omar Sarai wa chama cha UDA.
Katika maeneo ya Changamwe, Jomvu na Nyali, Sarai aliongoza utafiti huo huku takwimu za jumla zikionyesha akiungwa mkono kwa asilimia 51.8 kote kaunti ya Mombasa, Abdulswamwad Sharif Nassir wa ODM akiwa na asilimia 32.8 huku Dkt William Kingi wa chama cha PAA akifuatia kwa asilimia 4.2
Kulingana na Dzombo, utafiti huo unawaweka Sarai na Nassir kama wapinzani wakubwa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Mombasa, huku chama cha UDA kikionekana kuyavunja makali ya chama cha ODM, licha ya kaunti ya Mombasa kuonekana kuwa ngome ya ODM.