Wakati wakulima, wafugaji, na wavuvi wanapokumbwa na mabadiliko makubwa ya hali ya anga, Radio Kaya kwa ushirikiano na BBC Media Action imejiweka katika mstari wa mbele wa kuhakikisha kuwa mwananchi anapata taarifa zitakazo mfaa katika kufanya maamuzi yake ya kila siku.
Kupitia kwa kipindi Ustawi kinachopeperushwa hewani kila siku ya Jumamosi mwendo wa saa moja na robo usiku Radio Kaya imekuwa ikipeana taarifa za hali ya hewa na mawaidha ya jinsi ya kujiendeleza kimaisha wakati huu ambapo ulimwengu unakumbwa na mabadiliko ya tabia nchi.
“Ustawi ndio muokozi wa mvuvi, mkulima na mfugaji. Kupitia kwa kipindi hiki napitisha ujumbe kwao kuhusu jinsi misimu itakavyokuwa na ni jinsi gani wanafaa kujipanga ili wasipate hasara,” amesema mtayarishaji wa kipindi hicho Dominick Mwambui.
Mwambui ameongezea kuwa yupo na jukumu kubwa ikizingatiwa kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi humtegemea sana ili awapashe habari kuhusu jinsi hali ya hewa itakavyokuwa.
“Wakati mwingi inanibidi nitumie muda mwingi hata kukesha nikijaribu kurahisisha taarifa kutoka kwa wanasayansi ili ieleweke kwa urahisi na msikilizaji. Hili si jambo rahisi lakini najitahidi nakukomaa kila siku. Furaha yangu kuu ni pale ninapokamilisha kipindi kwa muda ufao, pia pale unapopokea ujumbe kutoka kwa msikilizaji kuhusu kipindi,” amesema Mwambui.
Hata hivyo ameelezea wasiwasi kuhusiana na kipindi cha Ustawi na kuwaomba wahusika katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji kuwa na urahisi wa kupeana taarifa.
“Mafanikio ya kipindi hiki sio mafanikio kwa Radio Kaya wala BBC Media Action bali ni mafanikio kwa mwananchi, mananchi anapoweza kujiendeleza kwa kuelewa vyema hali ya hewa basi tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana katika kuhakikisha tupo na usalama wa chakula na rasilimali tunazoweza kuzitegemea kwa muda mrefu, tunapokwamilia na taarifa maofisini hilo ni kosa kubwa sana,” ameongezea Dominick.
Sikiliza kipindi ustawi kila siku ya Jumamosi saa moja na robo usiku.