Story by Our Correspondents-
Huku wakaazi wa maeneo manane nchini ikiwemo kaunti za Mombasa na Kakamega wakishiriki uchaguzi wa ugavana na ubunge, idara ya usalama imeahidi kudumisha usalama katika maeneo yote kipindi chote cha uchaguzi.
Idara hiyo imesema maafisa wake wa usalama wamejipanga vyema kuhakikisha wakaazi wanalindwa hadi mashinani ili kuhakikisha uchaguzi wa ugavana wa kaunti hizo unafanikishwa vyema.
Nayo Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kupitia Afisa mkuu wa uchaguzi katika kaunti ya Mombasa Swalha Yusuf amesema zoezi la uchaguzi katika kaunti hiyo limeanza vyema huku usalama ukiimarishwa katika kaunti nzima ya Mombasa.
Wakati uo huo wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo bunge mbali mbali ya Mombasa wakiongozwa na John Ole Taiswa anaesimamia eneo la Nyali, wamesema wana imani kwamba shughuli ya kuhesabu kura vituoni itakamilika mapema.
Ole Taiswa amesema wameeka mipangilio yote ya kuwatambua wapiga kura sawa na jinsi ya kuweka alama kwa wale ambao tayari wameshiriki upigaji kura wa awali wa Agosti 9.