Story by Mimuh Mohamed-
Wizara ya mazingira na misitu nchini imeliagiza shirika la kuhifadhi kisitu nchini KFS kufutilia mbali leseni ya kusafirisha miti ya mbuyu kutoka kaunti ya Kilifi na kuuzwa nchini Marekani hadi pale kesi iliyowasilishwa mahakamani na mamlaka ya mazingira nchini NEMA ya kupinga biashara hiyo itakapoamuliwa.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Waziri wa mazingira na misitu nchini Soipan Tuya, amesema amefanya mazungumzo na Waziri wa uchukuzi nchini na kukubaliana kuzuia usafirishaji wa miti ya mbuyu nje ya nchi hadi pale pande husika zitakapoafikiana.
Soipan aidha ameeleza kwamba tayari amepokea barua rasmi kutoka kwa mamlaka ya NEMA iliyofutilia mbali leseni ya kung’olewa kwa mibuyu, akisema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya maafisa wa wizara hiyo watakaokosa kuzingatia utaratibu ufaao juu ya shughuli hilo.
Soipan hata hivyo amewahakikishia wakenya kwamba serikali inaendeleza jitihada kuongeza kiwango cha misitu hadi asilimi 30 kwa kipindi cha miaka 10 kwa kupanda miti bilioni 15 katika kipindi hicho.