Wakaazi wa Kaunti ya Mombasa na viungani mwake wanazidi kuhangaika kwa juma la pili sasa, huku Maafisa wa trafiki wakiimarisha msako wa magari ya uchukuzi wa umma yanayokiuka sheria za trafiki nchini.
Mshirikishi mkuu wa Chama cha Wamiliki wa matatu Kanda ya Pwani Salim Mbarack Salim amesema kwamba hali hiyo itatatuliwa pale sheria zinazofungamana na sekta ya uchukuzi wa umma nchini zitakapopigwa msasa.
Akizungumza Mjini Mombasa, Mbarack amesema kwamba baadhi ya sheria hizo ikiwemo kumtia nguvuni mmiliki wa matatu kutokana na makosa ya Dereva au Kondakta ni dhalimu na ni sharti ziondolewe kabla ya wahudumu hao kurudisha huduma za uchukuzi wa umma barabarani.
Mbarack vile vile amedokeza kwamba kwa juma la pili sasa, Maafisa wa trafiki wamekuwa wakiwahangaisha wahudumu wa matatu licha ya kutimiza masharti hitajika na akazitaka pande zote mbili kutekeleza majukumu yao bila ya mfarakano.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.