Picha Kwa Hisani – Freyzee FaceBook Account
Baada ya kimya cha miaka miwili, mwanamuziki kutoka kaunti ya Lamu, Freyzee amezindua ngoma yake mpya kwa jina ‘Badilisha.’
Hii ni baada ya mashabiki wake kushangaa alikokwenda na kumuulizia kwa muda mrefu kupitia mitandao ya kijamii.
Wasanii wengi wamejitokeza na kumpongeza kwa ujio wake mpya kupitia ngoma yake hiyo iliyotengenezwa na mzalishaji muziki maarufu kutoka Mombasa Emmy Dee.
Freyzee ambaye alitamba na wimbo wake ‘Utanipenda’ uliorekodiwa na mzalishaji muziki Shirko, ameonyesha kutokata tama kutokana na hali ngumu aliyokuwa anapitia tangu ujio wa janga la corona na kurudi kwenye tasnia ya muziki kwa kishindo kikuu.
‘Utanipenda’ ndio wimbo uliomtambulisha kwa mashabiki na kumfanya avume ndani na nje ya Pwani. Tetesi za kila aina zilizuka mitandaoni baada ya kupotea kwake kwenye sanaa na hata mitandaoni tangu mwishoni mwa mwaka wa 2019.
Aidha, msanii huyo ametoa shukrani zake kwa mashabiki na wanamuziki walioipa shavu ngoma hiyo.
Unaizungumziaje ngoma hii mpya kutoka kwa Freyzee?