Meneja wa Mamlaka ya barabara za mashinani yaani ‘Kenya Rural Roads Authority’ katika kaunti ya Kilifi Mhandisi Benson Masila amesema kuboreshwa kwa miundo msingi katika kaunti ya Kilifi kutaimarisha shughuli za biashara katika kaunti hiyo.
Masila amesema kufunguliwa kwa barabara ya kutoka Mariakani hadi bamba iliyo na umbali wa kilo mita 45 tayari umeleta mabadiliko katika sekta ya biashara huku akidai kuwa ujenzi wa barabara nyingine ya umbali wa kilomita 6 kutoka Kilifi hadi Kiwandani vile vile umebadilisha pakubwa shughuli za uchukuzi.
Akizungumza kule Bamba katika kaunti ya Kilifi, Masila amesema mbali na barabara hizo, ujenzi wa barabara ya umbali wa kilo mita 36 kutoka eneo la Marikebuni hadi Marafa unaelekea kukamilika.
Masila vile vile anaitaja barabara ya Malindi- Sala gate ya gharama ya shilingi bilioni 5.6 ya umbali wa kilo mita 121 kama itakayoimarisha zaidi shughuli za kiuchumi na biashara katika maeneo hayo.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.