Story by Our Correspondents
Uharibifu wa misitu ya Kaya na unyakuzi wa ardhi ndio chanzo kikuu kinachokandamiza uhuru wa kuabudu kwa jamii ya wamijikenda.
Haya yamebainika katika kikao cha kuangazia uhuru wa kuabudu kilichoandaliwa na Shirika la Search For Common Ground likishirikiana na Coast Interfaith Council of Clerics CICC katika eneo la Kinondo kaunti ya Kwale.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu wa Kaya Tiwi Salim Mwasibu amesema ili kuafikia uhuru wa kuabudu na kuendeleza amani baina ya dini mbali mbali kuna haja ya misitu ya Kaya kulindwa sawa na kuzuia unyakuzi wa ardhi.
Naye Mohamed Ali Sibabu kutoka Kaya Simila eneo la Pungu amesema changamoto hizo zimechangiwa na wazee wa Kaya kutoshirikiana.
Kwa upande wake Afisa wa miradi kutoka Shirika la Search For Common Ground, Zena Hassan, amesema changamoto hizo ni miongoni mwa mambo wanayolenga kutatua kupitia mradi wanaoutekeleza katika kaunti za Kilifi, Mombasa, Tana River, Lamu, Garissa na Nairobi unaofahamika kama JISRA.
Zena hata hivyo ameihimiza jamii kuendeleza uhuru wa kuabudu ili kuepuka mizozo baina ya dini mbali mbali na kuendeleza uwiano na amani katika jamii.
Kauli yake imeungwa mkono na Naibu Kamishna wa gatuzi dogo la Matuga Lucy Ndemo aliyewahakikishia wazee hao kwamba serikali inajitahidi kuhakikisha maeneo yaliyo na umuhimu wa kitamaduni kulingana na katiba ya nchi yanalindwa.