Picha kwa hisani –
Kiongozi wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP) Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine ameondoa mashitaka yake ya kupinga uchaguzi wa Urais wa Uganda aliyowasilisha dhidi ya Rais Yoweri Museveni.
Bobi wine ameitaja hatua ya jaji kukataa kuongezea ushahidi zaidi uliowasilishwa na timu yake kama sababu ya kuondoa kesi hiyo.
Pia ameongezea kuwa suala hilo litaamuliwa na wananchi lakini akatoa wito kwa wafuasi wake kutojihusisha na ghasia.
Hatua ya Bobi Wine inakuja siku moja baada ya Rais Museveni, Tume ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu kuwasilisha hati zao za kiapo 185 kujibu sababu 53 ambazo timu ya wanasheria ya Bobi Wine ilikuwa imeibua kuthibitisha kuwa uchaguzi huo ulikuwa wa wizi, na haukuwa huru na wa haki.
Chama cha Rais Museveni pia kimetuma ujumbe wa Twitter kuwa Museveni amepata ushindi katika kesi hiyo.
Siku ya Jumapili mawakili wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) walisema Bobi Wine atakabiliwa na athari kubwa za kifedha ikiwa atathubutu kuondoa ombi la kupinga ushindi wa Museveni kwenye Mahakama Kuu.