Taarifa na Salim Mwakazi.
Kwale, Kenya, Julai 18 – Serikali kupitia wizara ya madini inalenga kuanzisha utafiti kubaini iwapo uchimbaji madini umesababisha ugonjwa wa saratani miongoni mwa wakaazi waliokaribu na maeneo yanayochimbwa madini na kampuni ya Base Titanium kama inavyodaiwa.
Akizungumza katika eneo la diani kaunti ya Kwale katibu katika wizara ya madini nchini John Omwenge amesema kuwa tetesi hizo zinazoibuliwa na wakaazi ni tata na zifaa kuchukuliwa kwa uzito.
Afisa katika kampuni ya Base Titanium, Pius Kassim amesema tetesi hizo hazina ukweli kwani kampuni hiyo ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa uchimbaji madini unaendelezwa na kampuni hiyo hauna madhara ya kiafya kwa wakaazi.
Naye mkurugenzi mtendaji wa shirika la Transparency International Samuel Kimeu amesema wanalenga kuleta pamoja mashirika yanayohusika na masuala ya madini ili kuhakikisha kuna usawa katika suala la fidia na uhamisho wa waathiriwa.
Wameyasema haya huko Diani wakati wa uzinduzi wa kamati nne zitakazoshughulikia masuala tata yanayohusiana na shughuli za uchimbaji madini ikiwemo masuala ya ardhi, fidia za waathiriwa, athari za kiafya na maswala mengine.