Story by: Mimuh Mohamed
Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi umetoa tahadhari ya kutokea kwa shambulizi la kigaidi humu nchini na kuwataka raia wa Marekani kuwa waangalifu wanapokuwa katika maeneo ambayo raia wa kigeni huzuru kwa wingi.
Katika tahadhari hiyo iliyotolewa ubalozi huo wa Marekani humu nchini umesema jiji la Nairobi bado ni eneo linalolengwa zaidi na magaidi ambao wanapanga kutekeleza mashambulizi.
Ubalozi huo wa Marekani umewataka wakenya pamoja na raia wa Marekani kuwa waangalifu na mazingira yao huku ukipongeza serikali ya Kenya kwa kuongeza juhudi za kukabiliana na mitandao ya kigaidi.
Notisi hiyo imebainisha kwamba makundi ya kigaidi yanaweza kufanya mashambulizi pasi na kutoa ilani, yakilenga hoteli, majengo ya ubalozi, mikahawa, shule, vituo vya polisi, nyumba za ibada na maeneo ambayo watalii huzuru mara kwa mara.