Picha kwa hisani –
Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetoa tahadhari ya ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa corona.
Katika taarifa yake iliyotumwa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, ubalozi huo, umesema kuwa kumekua na taarifa za ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini Tanzania tangu mwezi Januari.
Ubalozi huo pia unasema hospitali na vituo vya afya nchini Tanzania vinaweza kuzidiwa kwa haraka na idadi ya wagonjwa.
Taasisi mbalimbali zimeendelea kutoa tahadhari ya maambukizi ya virusi vya corona.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Tanzania (SUA) ilitoa taarifa hapo jana kwa wanafunzi na wafanyakazi wake kujilinda dhidi ya maambukizi ya corona.
Nacho Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kilitoa waraka wa kuchukua tahadhari ya kujilinda na maambukizi ya corona.
Mwezi uliopita Kanisa Katoliki nchini Tanzania pia lilitoa tahadhari juu ya wimbi jipya la maambukizi ya corona na kuwataka wananchi kuchukua hatua zote za kujikinga.
Hata hivyo Wizara ya afya nchini humo bado haijathibitisha taarifa za uwepo wa wagonjwa au vifo vinavyo sababishwa na wimbi jipya la virusi vya corona.
Mara ya mwisho kutolewa kwa taarifa za mwenendo wa maambukizi ya virusi vya corona nchini Tanzania ilikua mwezi Aprili mwaka uliopita.