Picha kwa hisani –
Katibu mkuu wa muungano wa wafanyikazi nchini COTU, Francis Atwoli amesema atachukua jukumu la kushtaki Waziri wa Afya nchini Mutahi Kagwe kwa kushindwa kutatua matakwa ya wahudumu wa afya nchini.
Atwoli amesema Kagwe amezembea kuwajibikia majukumu yake kama Waziri wa Afya nchini na kutazama wakenya wakiendelea kuhangaika kufuatia wahudumu wa afya kushiriki mgomo uliodumu kwa mwezi mmoja sasa.
Atwoli amesema hatua atakayoichukua itasaidia pakubwa wananchi wanaohitaji hudumu za kiafya huku akisema Rais Uhuru Kenyatta pia anafaa kuchukua hatua za kinidhamu kwa Waziri waliozembea kuwajibikia majukumu yao kama Kagwe na kuwafuta kazi.
Wakati uo huo amedokeza kuwa Wizara ya Afya, ile ya Leba na baraza la magavana wameendelea kukiuka haki na uhuru wa vyama vya wafanyikazi hasa sekta ya afya, akisema ni lazima viongozi kuwajibikia majukumu yao.
Hata hivyo ameshikilia kuwa fedha zinazosambazwa kwa vyama vya wafanyikazi ili kutetea maslahi ya wafanyikazi ni fedha za wafanyikazi na wala sio za serikali kwa hivyo serikali na idara husika zinajukumu la kutatua matakwa ya wafanyikazi.